WANAFUNZI ELIMU YA JUU WATAMBUE MAVAZI
NI SEHEMU YA MAADILI
HIVI karibuni kulitolewa taarifa za kupiga marufuku uvaaji wa mavazi
ambayo ni kinyume cha maadili kwa vijana wa kitanzania.Ni baada ya uongozi wa
Chuo cha Biashara (CBE) kuwatolea uvivu baadhi ya wanafunzi katika kampasi zake
kwa kutoa onyo kali na kutowaruhusu kuingia katika eneo la kitaaluma. Ni
matumaini yangu kwamba taarifa iliwafikia ipasavyo walengwa kuhusu maadili ya namna ya uvaaji kwa wanafunzi
wa vyuo.
Hii ilitokana na kukithiri kwa
uvaaji holela wa mavazi yasiyo rasmi, hivyo baadhi ya wahadhiri wa chuo hicho
kulalamikia suala hilo. Baada ya uongozi wa chuo kubaini kumekuwapo na
ukiukwaji wa maadili, kutumia vibaya uhuru wa uvaaji mavazi waliopewa na
kupelekea wakati mwingine kuingia darasani na mavazi yasiyo rasmi. Uongozi wa chuo hicho ndipo ukaamua wanafunzi kuvaa mavazi rasmi na kwamba ambaye hatakuwa tayari kufuata
utaratibu huo uliowekwa atasimamishwa masomo kwa takriban miezi mitatu na
mwanafunzi atakayefika maeneo ya chuo akiwa hajavaa mavazi hayo rasmi hatoruhusiwa
kuingia katika eneo la chuo.
Hii ni taarifa nzuri kwa vijana
hasa wale ambao wanatarajia kujiunga na vyuo vikuu na wale walio katika elimu
za chini kama msingi na sekondari. Iwapo uamuzi huu utatekelezwa vizuri ni
dhahiri kwamba wanafunzi watakaojiunga na vyuo nao wataukuta utaratibu huo na
watauendeleza. Hii itawawezesha kuzoea uvaaji huo wa mavazi rasmi na kuwa
utamaduni wa wanafunzi wa vyuo na taasisi nyingine za elimu.
Mara nyingi nimekuwa najiuliza
kwa nini vijana wengi wapo nje ya
maadili. Je, ni kukosa elimu stahili juu ya maadili au ni kujifunza maadili ya
watu wa Magharibi kwani ni kweli kwamba mambo wanayoyafanya vijana kwa sasa ni maeneo
mengi yameathiriwa na uigaji kutoka tamaduni za mataifa yaliyoendelea.
Labda tufunguane macho na fikra
juu ya suala hili la maadili, kwa kuiangalia tu maana ya maadili wewe kama
kijana uaweza ukajua ni wapi unakosea na wapi haukujifunza tangu ukiwa mtoto
hadi kufikia umri ulionao hivi sasa. Jifunze sasa…Ni dhahiri kwamba, Maadili ni
mafundisho na mwongozo yanayopatikana sehemu mbalimbali na katika nafasi
mbalimbali kama vile katika malezi,
lengo likiwa ni kutaka kumuelekeza binadamu atende kwa namna ambayo
itamjenga yeye pamoja na jamii nzima inayomzunguka na kwamba maadili katika
jamii ni yale yale ila yanaweza
kutekelezwa kwa namna tofauti kutokana na mazingira tofauti. Je wewe kijana
ulikuwa unajua hilo?
Labda turudi nyuma enzi za mababu
zetu ambako ni dhahiri kwamba kuna utofauti kati ya ‘ukale na usasa’. Hapo
awali enzi za mababu zetu tunaona kuwa maadili yalikuwamo na yalikuwa
yanatolewa kwa namna maalumu kulingana na imani ya dini, utamaduni wa sehemu
fulani au hata falsafa na taratibu za kimaisha za jamii fulani. Kumfundisha mtoto
maadili ilikuwa ni jambo muhimu kwani ilimuandaa kuwa imara wakati atakapofikia
umri wa yeye mwenyewe kujitegemea katika maisha. Pia ilimsaidia katika kujua
mabaya na mazuri yanayomzunguka ikiwa ni pamoja na adabu na hekima ndani ya
jamii yake.
Chanzo cha kupotea kwa maadili kwa mtazamo wangu
naona ni kutokana na huu utandawazi ambapo ni wazi sayansi na teknolojia zimekuwa
kwa kasi na hivyo kuwaathiri watumiaji ambao kwa kiasi kikubwa ni vijana. Ni
dhahiri kwamba uwepo wa teknolojia hizi ambazo ni pamoja na runinga, kompyuta,
simu na nyinginezo, ndizo zilizosababisha kupoteza kabisa maadili ya vijana wa
Kiafrika.
Katika suala la uvaaji sidhani kama kuvaa milegezo
na kusuka nywele kwa wanaume ni asili ya Mwafrika, pia uvaaji wa nusu uchi na
kupita mbele za watu tena bila ya kuwa hata na chembe ya uoga ni utamaduni wa Mwafrika.
Huku ni kuiga tu kwa wenzetu wa Mataifa ya Magharibi
hasa Ulaya na Marekani. Tujivunie uafrika wetu na kuvaa mavazi yetu ya asili na
kuacha kuwaiga. Hivi hatujiulizi kwamba wao hawaigi mavazi yetu? Kama hujui basi achana na mazoea ya kuiga mavazi
yao na tuvae mavazi ya kwetu kwani kwa kipindi hiki wao ndiyo wanaoiga uvaaji
wa mavazi ya kiafrika na kuachana na mavazi yao. Huoni kama ni jambo la
kujivunia kwa Waafrika? Chunguza baadhi ya Wasanii, watu maarufu wa Marekani na
Ulaya na watalii wanaofika katika nchi yetu utapata jibu.
Baadhi ya mavazi hayo ni mavazi ya kitenge, batiki
na khanga na wanatamani sana yawe ndiyo mavazi yao ya asili.
Mi naona tunataka tuipuuze asili yetu ya tulikotoka,
kama wao wana asili yao kwa nini na sisi tusiitukuze asili yetu Waafrika?
Elimu tunayoipata darasani tukichanganya na maadili
kutoka kwa waliotutangulia na tukiyazingatia ni wazi tutafika kule tuendapo na
kuwa kama kioo cha wadogo zetu wanaotufuata. Tukianza sisi leo kama tulivyoyakuta
kwa waliotutangulia ni wazi kwamba hata wadogo zetu watayaendeleza na kurudisha
ustaarabu wa Kiafrika unaosifika kwa maadili mazuri.
Kama Serikali inavyofanya mchakato wa kutafuta Vazi
la Taifa, inapasa hata katika Taasisi za Elimu kutumia mavazi hayo ili
kuwatambulisha na kuwatofautisha wanafunzi wa watu wengine na hii itasaidia katika kuujenga upya utamaduni wa Mtanzania
ambao umekuwa ukipotea siku hadi siku kutokana na uingiaji wa sayansi na
teknolojia.
Tunaweza tukiamua,vijana tuamke na tuzingatie
maadili yaliyo bora,tujiheshimu katika uvaaji, kwani kuiga ni ushamba tofauti
na jinsi wengi wanavyodhani kwamba kuvaa mavazi ya asili ni ushamba na kuiga ni
kwenda na wakati.
GET UP YOUTH
Tusisahau tulikotoka kwa kuiga ya mbele...tutapotea....GET UP.
ReplyDelete