Thursday, June 21, 2012

MIAKA 48 YA MUUNGANO

MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR NI KICHOCHEO  MAENDELEO YA KISWAHILI  ULIMWENGUNI

Ikiwa imepita miaka 48 tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane na kuunda Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, masuala yanayozungumziwa sana katika Muungano huu kwa sasa ni masuala ya Katiba Mpya na Siasa. Tumesahau kwamba Muungano huu ndiyo uliozaa Jamhuri na kuitengeneza hiyo Katiba ambayo hii leo imeundwa Tume ya kupitia maoni ya Watanzania ili kupata Katiba Mpya.
Jambo la kukumbuka ni namna lugha yetu adhimu ya Kiswahili ilivyotumika kama . Ni Kiswahili ambacho ndicho kilileta changamoto za muungano huu kwani wa leo hii. Tukumbuke kwamba Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hayati Aman Abeid Karume walitumia Kiswahili katika kuuunganisha watu wa mataifa haya mawili na kuwa kitu kimoja kama Watanzania.
Leo hii mifumo yetu ya elimu inaonyesha haikipi nafasi Kiswahili kwa upana wake. Kiswahili kinachukuliwa ni lugha ya kishamba na kuzitukuza lugha za kigeni kama vile Kiingereza na Kifaransa. Watu hulazimika hata kutoa pesa nyingi ili tu waweze kuzijua lugha hizo na kusahau umuhimu wa lugha yao. Hivi huku ndiyo kukitangaza Kiswahili au kukididimiza?
Kwa nini hatuna uzalendo na lugha yetu. Vijana wengi utawakuta hata kwenye mazungumzo yao ya kawaida wanatumia zaidi Kiingereza ambacho nacho ni kibovu. Kila mtu anataka aonekane kwamba anakijua zaidi ya mwenzake. Kwani ukizungumza lugha yako haueleweki? Mtu yupo radhi achanganye misimbo ili mradi tu. Tumekua watu wa kuthamini  tusichonacho kuliko kile tulichonacho.
Jamii hivi sasa imeathirika na wengi tunakichukulia Kiingereza kama lugha ya wasomi. Hii ni dhahiri kwa watu wengi ambao wakifika majumbani kwao hasa wa sehemu za vijijini hawatumii tena hata zile lugha zao za asili kwa kuwa ametoka masomoni, hivyo kutafuta utofauti kati yake na watu aliowakuta huko. Anachotaka yeye ni ile hali ya kujiona amesoma kuliko mtu yeyote hapo kijijini.
 Kwa nini tunasahau tulipotoka. Sisi ni Watanzania na tuliamua kwa pamoja kukitumia Kiswahili kama Lugha ya Taifa. Sasa inakuaje tukidharau. Hatuoni kama tunajidharau wenyewe na kukiona Kiswahili kama si cha kwetu Watanzania. Ina maana maamuzi tuliyoyachukua na kuamua kukifanya Kiswahili kuwa lugha yetu ya Taifa tulikosea au tulilazimishwa. Sidhani kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipitisha kuwa Lugha ya Kiswahili itumike kama Lugha ya Taifa alikosea!. Kama kulikuwa na watu wa kupinga mbona hawakujitokeza wakakubaliana na matakwa yaliyotolewa. Leo hii tunavyokidharau inamaanisha kuwa Kiswahili hakina haja ya kuendelezwa? Tafakari!

 Mwandishi ni mtaalamu wa  lugha.